19 Machi 2011 - 20:30

Baada ya mjadala wa mwezi mmoja na mashinikizo ya kila upande, hatimaye Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO limeipatia Palestina uanachama kamili. Shirika hilo ambalo makao makuu yake yapo mjini Paris Ufaransa jana lilipigia kura ombi la kupatiwa Palestina uanachama katika shirika hilo.

Ripoti ya ABNA- Nchi wanachama 107 zilipiga kura ya ndio, 14 kura za hapana na wanachama wengine 52 wakijizuia kupiga kura. Kama ilivyotarajiwa Marekani ilipiga kura ya hapana ikipinga Palestina kupatiwa uanachama katika Shirika la UNESCO. Katika radiamali yake ya kwanza, Marekani imetangaza kukata misaada yake kwa Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO. Aidha imesema, hata fedha ilizokuwa imeahidi kulipatia shirika hilo mwishoni mwa mwezi huu haitofanya hivyo. Uanachama wa Palestina katika UNESCO unahesabiwa kuwa ushindi wa kidiplomasia kwa Palestina, hasa katika kipindi hiki ambapo ulimwengu unasubiri kwa hamu uamuzi wa ombi la Wapalestina la kutaka kutambuliwa rasmi nchi yao.